January 24, 2015

 Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ametangaza rasmi kujiuzulu wadhifa wake hii leo kufuatia kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow.
Prof. Muhongo ametangaza uamuzi huo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika makao makuu ya wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es salaam.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu uamuzi wake kutokana na shinikizo au la, Prof Muhongo amesema huo ni uamuzi wake binafsi baada ya kushauriana na familia yake pamoja na viongozi wenzake kutokana na kunyooshewa vidole kwa kiasi kikubwa, kwa hiari yake binafsi amefikia uamuzi huo.
Kuhusu nafasi yake ya ubunge ambao ni wa kuteuliwa na Rais, Prof Muhongo amesema kuwa bado ataendelea kuwa mbunge kwa kipindi kilichobakia.
Prof. Muhongo anaungana na Mwanasheri Mkuu wa Serikali Fredrick Werema ambaye alijiuzulu kwa kashfa hiyo pamoja na Waziri wa Ardhi Prof. Anna Tibaijuka aliyeombwa kuachia ngazi kutokana na kashfa hiyo.
Kufuatia hatua hiyo mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Mh Zitto Kabwe amepongeza uamuzi huo wa Prof Muhongo ambapo amesema kuwa kuwa hatua hiyo ni heshima kubwa kwa bunge.
"Napenda kuchukua nafasi hii kutambua busara aliyochukua ambayo naamini itasaidia harakati za kujenga demokrasia yenye uwajibikaji. Naamini uamuzi wa Ndugu Muhongo umewezesha kulinda heshima ya Bunge na maazimio yake. Kwa muda mfupi alioongoza Wizara hiyo, Ndugu Muhongo ameweza kuongoza mabadiliko kadhaa muhimu ya kiutendaji katika wizara hiyo na taasisi zake. Hata hivyo, nafasi ya Wizara aliyokuwa anaongoza katika suala la Tegeta Escrow imemtia doa kubwa ambalo ilikuwa lazima awajibike. Naamini Rais Kikwete atamteua mtu mchapakazi na makini zaidi atakayeweza kuendeleza yale mazuri ya Ndugu Muhongo na kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza." Amesema Zitto kupitia ukurasa wake wa Facebook.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE